Call for Interview

Placements

Visitors Counter

»Online   35        
»Today   369       
»Yesterday  5123       
»Week   31165        
»Month   99053       
==================
»Total 21570462        

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

August 16, 2016


     

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tathmini ya Ukasimishaji wa Madaraka ya uendeshaji wa mchakato wa Ajira kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Hivi karibuni Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilifanya  marekebisho  ya  Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka 2002 kupitia “Written Laws” (Miscellaneous Amendments) Na. 2 ya Mwaka 2013 Ili kukidhi mahitaji ya sasa ya Serikali ambapo kifungu cha 29(A) (1) kiliongezwa na kufanyiwa marekebisho ambapo Katibu wa Sekretarieti ya Ajira amepewa uwezo wa kukasimu Madaraka (delegate) kwa Afisa Mtendaji Mkuu au kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kuendesha  mchakato wa Ajira.

Kufuatia Utaratibu huo ambao ulitangazwa katika Gazeti la Serikali namba 70 la tarehe 14 Machi, 2014 ambalo liliainisha jumla ya kada 22 kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa ili kusogeza huduma karibu na wananchi pamoja na kurahisisha zoezi la upatikanaji wa watumishi katika Mamlaka husika. Kada ambazo zimekasimiwa ni Mchapa Hati Daraja la II, Msaidizi wa Maktaba  Daraja la II, Mkaguzi wa Mji ,Mwandazi  Daraja la II, Mhudumu wa Jikoni, Afisa Maendeleo ya Jamii Msaidizi Daraja la III, Dereva Daraja la II, Dereva Mitambo Daraja la II, Katibu Mahsusi Daraja La III, Msaidizi wa Kumbukumbu (Nyaraka) Daraja La II ,Mpokezi, Msaidizi wa Ofisi, Mlinzi, Fundi Sanifu Msaidizi, Afisa Mtendaji wa Kijiji Daraja la III, Afisa Mtendaji wa Mtaa Daraja la II, Afisa Mtendaji wa Mtaa Daraja la III, Mlezi wa Watoto Msaidizi, Nahodha Daraja la II, Polisi Msaidizi, Mhudumu Wa Boti Daraja la II pamoja na Muundaji Boti Daraja la II.

Tangu utekelezaji wa jukumu hilo mwezi Julai, 2014 hadi Desemba, 2015 jumla ya nafasi za kazi 2,011 zimetangazwa na jumla ya maombi 52,435 yalipokelewa. Katika Maombi hayo wasailiwa walioitwa kwenye usaili wa mchujo walikuwa 21,602 na wasailiwa waliofaulu katika hatua ya usaili wa mahojiano ni 5,904 katika saili 96 zilizofanyika katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Aidha katika nafasi hizo zilizotangazwa jumla ya waombaji 1,881 walishapangiwa vituo vya kazi na nafasi 130 ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Aidha, nawataka waajiri wote katika Utumishi wa Umma Nchini kutotumia Mamlaka yao vibaya na wazingatie misingi ya Utawala Bora ikiwemo Sheria, Kanuni na Taratibu katika Kutekeleza majukumu yao. Watekeleze mchakato wa Ajira kwa haki bila kutoa au kupokea Rushwa, pasipo upendeleo wowote ule kwa kuwa atakaebainika kwenda kinyume sitamvumilia, atawajibika kwa mujibu wa Sheria kwa kuwa watumishi wa Umma wapo ili watoe huduma kwa Wananchi.

Mwisho nimalizie kwa kutoa tahadhari kwa wananchi hususan waombaji wa  fursa za ajira Serikalini kujiepusha na wimbi la matapeli wanaowapigia simu na kutaka kuwatoza fedha ili kuwasaidia kupata ajira Serikalini. Ni vema watambue  kuwa ni kosa la Jinai kutoa ama kupokea Rushwa na wasikubali kurubuniwa na matapeli hao kwa kuwa Serikali haina utaratibu wa kudai fedha ili muombaji kazi apate kazi.

Ni vizuri ieleweke kuwa Serikali huendesha shughuli zake kwa mujibu wa Sheria, kanuni na taratibu hivyo wakipokea simu za namna hiyo ni vyema wakaripoti kwenye vyombo husika ikiwemo Polisi na Takukuru ili waweze kuwafuatilia matapeli hao na kuwachukulia hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.     

6 Januari, 2016.